To read this in English click here
Baba Askofu Emmanuel Joseph Makala wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria iliyoko mikoa ya Shinyanga na Simiyu ameanza matembezi ya hisani Jumapili ya wiki iliyopita na kutarajiwa kufika kilele tarehe mosi mwezi wanne mwaka huu wa 2018. Lengo la matembezi hayo ni kukusanya fedha kwaajili ya shughuli za misioni na maendeleo ya Dayosisi kwa ujumla.
Watu walioambatana na Kiongozi wa matembezi hayo ni pamoja Maafisa wa Dayosisi, Msaidizi wa Askofu Mchg. Trafaina Aseri Nkya, Katibu Mkuu Hapiness Yoram Gefi, Wakuu wa Majimbo, Watumishi toka Ofisi Kuu, Wachungaji, Wainjilisti, Wakristo wa Majimbo husika na wadau mbalimbali wa Dayosisi.
Aidha matembezi hayo yameanzia Usharika wa Neema ulioko Lamadi, Jimbo la Bariadi na kuelekea majimbo ya Meatu, Mashariki -Maswa, Kusini Kati – Mwadui, Kusini Mashariki – Kishapu, Shinyanga , Kanisa Kuu, Kusini Magharibi – Ushetu, Kasikazini Magharibi – Msalala na baadae kilele cha matembezi kufanyika Jimbo la Magharibi – Kahama.
Sambamba na matembezi hayo shughuli zingine zitakazokuwa zinafanyika ni kuiombea Dayosisi, kuhubiri habari njema, kutoa huduma kwa wahitaji na wale wenye kumbukumbu za kuzaliwa na ndoa, kubatiza watoto na watu wazima, kurudisha Wakristo kundini na Kubariki ndoa.
Baba Askofu alikaririwa akisema, “imefika wakati Dayosisi inatakiwa ibuni njia za kuweza kupata mapato ya ndani zaidi ya kutegemea ufadhili kutoka nje”.
Aidha fedha zitakazokuwa zimepatikana wakati wa matembezi zitatumika kununulia pikipiki kwaajili ya Wachungaji na Wainjilisti, Kulipa gharama za mafunzo kwa Wachungaji na Wainjilisti, kuezeka majengo ya kuabudia yaani Makanisa na kujengea nyumba za watumishi.
Pia wakristo wa Dayosisi wamepongeza uongozi wa Dayosisi kwa kubuni njia mbadala ya kupata mapato ya ndani kwakuwa kila Usharika utapata fursa ya kupokea matembezi na kupata huduma stahiki tena toka kwa uongozi wa juu wa Dayosisi.
Tukio hilo ni kubwa na la kihistoria toka kuanza kwa Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria mwaka 2012 na ambalo limegusa hisia za watu wengi nje na ndani ya Dayosisi. Hata hivyo wadau mbalimbali wameonesha nia ya kutaka kushiriki matembezi hayo kiroho kwa njia ya maombi na pia kimwili kwa njia ya kutoa sadaka, michango na vitu halisi ili kusaidia kufanikisha matembezi hayo ya hisani.